Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Malawi, Ban ataka wagombea na wafuasi waheshimu kazi ya kuhesabu kura

Uchaguzi Malawi, Ban ataka wagombea na wafuasi waheshimu kazi ya kuhesabu kura

Umoja wa Mataifa umetaka wagombea na wafuasi wao kwenye uchaguzi mkuu wa Urais, wabunge na serikali za mitaa nchini Malawi, kuheshimu kazi inayoendelea hivi sasa ya kuhesabu Kura.

Katibu Mkuu wa Umoja huo Ban Ki-Moon amenukuliwa katika taarifa akisema kuwa uchaguzi huo wa tarehe 20 Mei ulizingatia viwango kama ilivyoelezwa na taarifa za awali za waangalizi licha ya matatizo ya kiufundi yaliyojitokeza kwenye mchakato huo.

Hivyo ametaka wagombea, vyama vya siasa na taasisi za serikali kuwa na utulivu na kuiunga mkono tume ya uchaguzi ya Malawi ili ihitimishe kazi yake.

Amerejelea wito wake kwa wagombea na wafuasi kuheshimu mchakato unaoendelea wa kuhesabu kura na wafuat taratibu za kisheria kupatia suluhu manung’uniko yoyote yanayoweza kujitokeza.

Halikadhalika ametaka wazingatie azimio la Lilongwe la tarehe 10 Mei huku akiwasihi wafuasi wajiepushe na vurugu au vitendo vyovyote vinavyoweza kuharibu mchakato unaoendelea ambao amesema ni muhimu katika kuimarisha demokrasia nchini Malawi.