Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio kwenye bunge huko Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon (Picha:Maktaba)

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio kwenye bunge huko Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani shambulio la kujilipua kwenye jengo la Bunge huko Somalia, shambulio lililofanyika leo Jumamosi huku akisema hakuna mazingira yoyote ya kuhalalisha kitendo hicho.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akielezea mshikamano wake na wabunge wa Somalia, wake kwa waume ambao amesema ni wawakilishi wa wananchi na matumaini yao kwa mustakhbali wenye amani.

Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia wananchi wa Somalia, serikali na bunge lao wanapojitahidi kujenga amani na utulivu.

Halikadhalika amesifu hatua za haraka zilizochukuliwa na vikosi vya taifa vya ulinzi Somalia kwa ushirikiano na vikosi vya Afrika, AMISOM punde baada ya tukio hilo lililohusisha pia watu waliokuwa na silaha na ametuma rambirambi kwa familia za wafiwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Wakati huo huo wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani shambulio hilo wakisema kuwa ugaidi hauwezi kuhalalishwa kwa misingi yoyote ile.

Pamoja na kutuma rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia ahueni majeruhi wamerejelea wito wao wa kuendelea kupiga vita aina yoyote ile ya ugaidi wakisema kuwa watashirikiana na serikali ya shirikisho ya Somalia kudhibiti vitendo hivyo huku wakitaka wahusika wafikishwe mbele ya sharia.