Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yaendelea leo Bentiu, mtoto mmoja auawa baada ya kujeruhiwa kwa risasi: UNMISS

Kambini nchini Sudan Kusini wanokojihifadhi wakimbizi kufuatia mzozo unaoshuhudiwa nchini humo

Mapigano yaendelea leo Bentiu, mtoto mmoja auawa baada ya kujeruhiwa kwa risasi: UNMISS

Mapigano ya hapa na pale yaliyoanza mwisho mwa wiki kwenye maeneo mbali mbali nchini Sudan Kusini yameripotiwa kuendelea leo kwenye mji mkuu wa jimbo la Unity, Bentiu ambapo mtoto mmoja aliyekuwa anakimbia kuokoa maisha yake ameuawa.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari mjini New York kuwa mapigano hayo kati ya vikosi vya serikali, SPLA na wapinzani yaliripotiwa pia karibu na ofisi za ujumbe wa umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Amesema baada ya SPLA kudhibiti, pande kinzani ziliondoka eneo hilo na hali kutulia..

(Sauti ya Farhan)

Hata hivyo mapigano yaliibuka tena leo alfajiri karibu na kituo hicho yakihusisha silaha nzito na ndogo. Ujumbe huo umeripoti kuwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minne alifariki dunia kutokana na jeraha la risasi iliyokuwa imepoteza mwelekeo.

Hapo jana mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na upinzani yameripotiwa pia kwenye jimbo la Upper Nile huku baadhi ya makombora yakitua karibu na kituo cha UNMISS kilichopo eneo hilo.

Halikadhalika kwenye mji mkuu Juba UNMISS imesema kuliwepo na mapigano ya hapa na pale kati ya watu wa jamii ya Nuer wanaoishi kwenye kambi ya ujumbe huo na wale wa kabila la Dinka wanaoishi nje ya kambi hiyo. Hata hivyo polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya watu hao.

Wakati huo huo, mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Herve LAdsous amewasili Sudan Kusini akitokea Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ziara ya siku tatu kusisitiza jukumu la Umoja wa Mataifa katika ulinzi wa amani nchini humo.