Ban asikitishwa na hukumu ya kifo kwa halaiki Misri

28 Aprili 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ameeleza kusikitishwa na habari kuwa hukumu nyingine ya kifo ya halaiki imetolewa tena nchini Misri, kufuatia ya kwanza iliyotolewa mnamo Machi 24, 2014.

Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Ban amesema kuwa hukumu zinazoonekana bayana kuwa hazitimizi viwango wastani vya mashtaka ya haki, hususan zile zinazohusika na adabu ya kifo, huenda zikadhoofisha matumaini ya utulivu wa kudumu.

Amesema anatiwa wasiwasi na athari za hukumu kama hizo kikanda na kwa hali ya usalama, akiongeza kuwa utulivu nchini Misri ni muhimu kwa utulivu wa eneo zima la Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, Bwana Ban ameelezea kusikitishwa na uamuzi wa mahakama leo ambao umepiga marufuku shughuli za kundi la wanaharakati vijana la Aprili 6. Ameelezwa pia kukerwa na maamuzi ya mahakama ya rufaa kuthibitisha kifungo cha watu watatu maarufu kwa mchango wao katika mapinduzi ya mwaka 2011, wakiwemo waanzilishi wawili wa kundi la vijana.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter