Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ruzuku kwenye uzalishaji wa nishati itokanayo na kisukuku iondolewe: Wataalamu

Ruzuku kwenye uzalishaji wa nishati itokanayo na kisukuku iondolewe: Wataalamu

Jopo la wataalamu wanaokutana kwa siku mbili limesema kuwa uzalishaji wa nishati itokanayo na kisukuku imeathiri juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Watalaamu hao wanakutana chini ya mwamvuli wa mashirika ya kimataifa ukiwemo lile la Umoja wa Mataifa linalohusika na mazingira UNEP wamesema kuwa ili dunia iweze kupiga hatua kuondokana na matatizo ya tabia nchi lazima iteleze kwa vitendo mopango inayohusu gesi endelevu.

Wamebainisha kuwa moja ya jambo ambalo linapaswa kutiliwa mkazo na serikali zote ni kupunguza au kuondoa kabisa ruzuku katika uchimbaji au uzalishaji wa nishati itokanayo na kisukuku na kuwepo kwa mbadala wake kwa matumizi sahihi wa nishati ya gesi endelevu.

Wamependekeza pia kubiniwa kwa sera kwa vile imebainika moja ya kikwazo kinachorudisha nyuma juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni kutokana na kukosekana kwa sera imara zinaangazia eneo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Achim Steiner amesema kuna umuhimu wa kuibuliwa kwa sera akisema kuwa kukosekana kwake kumeifanya dunia ipoteze mwelekeo kwenye suala la nishati itokanayo na kisukuku.

Kwa hivi sasa UNEP inatekeleza mpango maalumu wa majaribio kuhusu sera mbadala katika nchi za Ghana, Kenya na Mauritius.