Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usalama wakumba utoaji chakula Sudan Kusini

Ukosefu wa usalama wakumba utoaji chakula Sudan Kusini

Shirika la Chakula Duniani WFP, litaendelea kusambaza chakula Sudan Kusini licha ya mashumbulizi yaliyotokea jana dhidi ya msafara wa chakula maeneo ya Malakal, ambapo meli nne zilipigwa na grenedi, na watu wanne kujeruhiwa

Elizabeth Byrs ambaye ni msemaji wa WFP, amesema kwamba hali ya usambazaji wa chakula ni tete, lakini mpaka sasa hivi vyakula vinafikishwa.

“ WFP na washirika wake wanjitahidi ili kudhibiti ukosefu wa usalama wa chakula. Sudan Kusini, hadi tarehe 22, mwezi April, zaidi ya watu 700,000 wamesaidiwa na chakula cha WFP kutokana na mzozo. Pia, kuna zaidi ya watoto 63,000 walio na umri chini ya miaka mitano ambao wamesaidiwa na chakula maalum maeneo ya Central Equatoria, Jonglei, Lakes, Unity, Upper Nile, Bahr el Ghazal Kaskazini na Warrap.”

Shirika la WFP limesema kwamba shida za usalama zinakumba shughuli zake, likiwa katikati ya zoezi la kuweka akiba ya chakula katika maeneo ambayo hayataweza kufikiwa kwa njia ya gari, mvua zikiendelea.

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limejadili juzi kuhusu mauaji yaliyotokea mjini Bentiu, wiki iliyopita, likikiri kutishwa sana na uhalifu huo. Limewaomba watekelezaji wawajibike. Kufuatia mkutano huo, leo msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kwamba Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, atawasili Sudan Kusini kesho kwa ajili ya uchunguzi wa mauaji hayo.