Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifaa vya kujikinga dhidi ya Ebola vyafika Guinea: WHO

Vifaa vya kujikinga dhidi ya Ebola vyafika Guinea: WHO

Shirika la Afya Duniani, WHO, limeanza kugawa vifaa vya kujikinga dhidi ya ugonjwa Ebola kwenye vituo vya afya, nchini Guinea.Taarifa ya Priscilla

(Taarifa ya Priscilla)

Zaidi ya tani Tatu na Nusu ya vifaa vimewasilishwa Conakry, mji mkuu wa Guinea, tarehe 30 mwezi Machi, zikiwemo nguo za kuvaa mara moja na madawa, kwa ajili ya kujikinga na maambukizo, na pia vifaa vya kuzika watu kwa njia salama.

WHO imekumbusha kwamba nusu ya walioambukizwa Conakry ni wafanyakazi wa afya, kwa hiyo kuwalinda na kuwapatia vifaa mwafaka ni lazima ili kudhibiti mlipuko wa Ebola.

Gregory Hartl ni msemaji wa WHO na anasema sasa hivi kuna visa 122 nchini Guinea, 7 Liberia, na watu 84 wameshafariki dunia kutokana na ugonjwa huu. Ameongeza visa huko Sierra Leone havijathibitishwa. Kwa jumla, amesisitiza kwamba mlipuko huu haufika kiwango cha hatari.

(Sauti ya Gregroy Hartl )

“ Kuna wafanyakazi wetu mjini Conakry, na tunaendelea kusambaa zaidi. Ugonjwa huu ni mbaya. Lakini, kitu nachotaka kuzingatia ni kwamba uambukizo wa mlipuko huu unafanana milipuko iliyopita. Kwa hiyo, jinsi ya kusitisha mlipuko huu ni kudhibiti maambukizo ndani ya hospitali, pia muhimu ni kufuatilia walioathirika na wale ambao bado hawajaenda hospitali na hawajui kwamba wameathirika, na kuwazuia kuambukiza wengine."

WHO inasema kuzuia maambukizo ndio njia ya pekee kujikinga na Ebola, kwa kuwa ugonjwa huu hauna dawa wala chanjo. Dalili za Ebola ni pamoja na homa kali, maumivu ya mishipa na kichwa, kuharisha na kutapika.

Mashirika ya madatkari wasio na mipaka, MSF na WHO yanaendelea kufanya kazi na Wizara ya Afya ya Guinea, ili kufuatilia visa vya Ebola, na kuandaa vyumba vya kutawisha wagonjwa ndani ya hospitali zote.