Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtandao wa Intaneti waweza kupunguza umaskini

Mtandao wa Intaneti waweza kupunguza umaskini

Mtandao wa Intaneti unaotumia kuhamisha-data kasi (broadband Internet) unafaa kuangaliwa kama nyenzo ya msingi ya kuleta maendeleo, kwa mujibu wa Kamisheni ya Maendeleo ya Kidigitali, iliyokutana mwishoni mwa wiki iliyopita, mjini Dublin, nchini Ireland.

Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo, Rais wa Rwanda Paul Kagame, amesisitiza umuhimu wa kihamisha-data kasi kwa kuinua uchumi wa nchi zinazoendelea, Aliongeza kwamba teknolojia za habari na mawasiliano, TEKNOHAMA au ICT, zinachangia katika kuimarisha sekta za elimu, afya, benki, na kadhalika kwa faida ya watu wote wakiwemo wanaoishi mashambani.

 Sauti ya Paul Kagame :

“ Kwa mfano, tumeona kwamba huko India, China au Brazil, mtandao wa Intaneti umechangia kwa zaidi ya asilimia 10 katika ukuaji wa uchumi kwa kipindi cha miaka mitano kilichopita. Afrika, tunakadiria kwamba Intanet inachangia kwa dola bilioni 18, ikitarajia kufika idadi ya dola bilioni 300 ifikapo mwaka 2025.”

Ili watu wote waweze kujiunga na mtandao unaotumia kihamisha-data kasi, washiriki wa mkutano huo wamesisitiza umuhimu wa kupunguza gharama za kujiunga na mitandao kwa kupitia ubia kati ya serikali na sekta binafsi, na kupendekeza mafanikio bora katika sekta hii. Uwekezaji mkubwa unahitajika kujibu mahitaji yanayotokana na ongezeko la idadi ya simu za mkononi zinazotumia Intaneti.