Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban yuko Ukraine, Šimonović awasili Crimea

Ban yuko Ukraine, Šimonović awasili Crimea

Harakati zote za kidiplomasia zinaendelea kutumika kupatia suluhu mzozo kati ya Ukraine na Urusi juu ya jimbo la Crimea ambapo hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Ukraine baada ya kukutana na viongozi waandamizi wa Urusi mjini Moscow siku ya Alhamisi akiwemo Rais Vladmir Putin. Taarifa zaidi na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Akiwa Kyiv mji mkuu wa Ukraine, Bwana Ban amekutana na Kaimu Rais Oleksandr Turchynov, na amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo kuwa amemweleza mzozo unaoendelea unaweza kusuluhishwa kwa njia ya mashauriano ya dhati pekee. Na zaidi ya yote amesema…

(Sauti ya Ban)

“Nimemweleza Kaimu Rais Turchynov hofu yangu lakini pia ninavyotiwa moyo na dalili ninazoona za kuongeza wigo wa ujumuishi, hususan nia ya kurejesha tena lugha ya Kirusi kama moja ya lugha rasmi Ukraine. Ujumuishi ni muhimu sana katika kurejesha utulivu kwenye nchi yenu.”

Na katika hatua nyingine Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki za binadamu Ivan Šimonović amewasili Crimea kwa ziara ya siku mbili ya kuweka msingi wa kazi ya jopo la watu wanne la Umoja huo la kufuatilia haki za binadamu kwenye eneo hilo.

Baadaye leo wakiwa Simferopol watakutana na wawakilishi mbali mbali wakiwemo wa taasisi ya uchunguzi na waandishi wa habari.

 Halikadhalika watakwenda Sevastopol na baadaye kurejea Kyiv. Wakati wa ziara yake ya awali mapema mwezi huu, Šimonović alitangaza kuundwa na kupelekwa mara moja kwa jopo la ufuatiliaji wa haki za binadamu Crimea.