Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM alazimika kuhitimisha shughuli eneo la Crimea, Ukraine

Mjumbe wa UM alazimika kuhitimisha shughuli eneo la Crimea, Ukraine

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa aliyekwenda kukagua hali ilivyo katika eneo la Crimea, Ukraine, amelazimika kuhitimisha ghafla shughuli zake katika eneo hilo kwa sababu za kiusalama, kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson.

Bwana Eliasson amesema kuwa Bwana Robert Serry, ambaye ni Mratibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mashariki ya Kati, alikutana na watu wasojulikana nje ya makao makuu ya jeshi la majini na kuamrishwa aondoke katika eneo hilo. Bwana Eliasson amewaambia waandishi wa habari kuwa baadhi ya watu hao walikuwa na silaha.

“Alienda kwa gari lake, na kukaa ndani ya gari, lakini gari hilo halikuweza kuondoka, kwa hiyo aliondoka kwa gari na kuanza kutembea kwenda hotelini. Akiwa njiani kuelekea hotelini, alisimama kwenye mgahawa na kunipigia simu. Kwa hiyo ripoti za hivi punde zaidi ni kwamba yupo kwenye mgahawa huo, akielekea hotelini, na sijui hoteli ipo wapi.”

Bwana Eliasson pia amesema hali mjini Kiev ambako yupo yeye ni tulivu kidogo, na amehisi kuna uungaji mkono wa dhati wa serikali ya sasa ya mpito. Ameongeza kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wamelazimika kuhamishwa kutoka eneo la Crimea katika siku chache zilizopita, na kwamba Bwana Serry ataweza tu kurejelea shughuli zake iwapo atahakikishiwa usalama.