Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo kuu la UM lizingatiwe kutatua mzozo wa Ukraine: Baraza la usalama laelezwa

Lengo kuu la UM lizingatiwe kutatua mzozo wa Ukraine: Baraza la usalama laelezwa

Saa 24 baada ya Baraza la Usalama kupatiwa muhtasari kuhusu hali ya usalama nchini Ukraine, mambo yamezidi kubadilika ikiwemo maeneo muhimu kwenye jimbo linalojitawala la Crimea nchini humo kama vile viwanja vya ndege, majengo ya umma na bunge la kikanda kushikiliwa na watu waliojihami wasiojulikana.

Huo ulikuwa ni ujumbe wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Baraza la usalama siku ya Jumamosi lilipokutana kwa faragha kujadili hali ya usalama Ukraine.

Amesema ripoti zaidi zinataja kuwa watu wenye silaha wasiojulikana wanadhibiti majengo ya utawala kwenye miji kadhaa mashariki na kusini mwa Ukraine.

Amesema kwa upande mwingine serikali mpya huko Crimea imeripotiwa kuomba usaidizi wa ulinzi kutoka Urusi lakini hata hivyo kuna habari njema kutokana na tangazo la serikali mpya ya Ukraine kutangaza azma yake ya kupanua wigo wa  ushiriki kwenye serikali ikiwemo kujumuisha wawakilishi kutoka Mashariki kwaUkraine.

Bwana Eliasson amewaeleza wajumbe hao kuwa huu ni wakati muhimu sana kurejelea lengo kuu la Umoja wa Mataifa ambalo wakati wote ni kuhakikisha migogoro na mizozo inapatiwa suluhu kwa amani na akasema hilo ndilo linapaswa kuwa mwongozo wa utatuzi wa kinachoendelea Ukraine.