Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji kwa misingi ya kikabila yanaendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mauaji kwa misingi ya kikabila yanaendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati

Raia huko Jamhuri ya Afrika ya Kati wanakabiliwa na ghasia za kupindukia kutoka kwa vikundimvya waasi vinavyochagiza mauaji ya kikabila huku wakitenda vitendo hivyo bila kuchukuliwa sheria yoyote, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kama anavyoripoti Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

Shirika hilo linasema maelfu ya waislamu wanaendelea kukimbia nchi hiyo kutokana na ghasia zinazochochewa na kikundi cha waasi kinachoungwa mkono na wakristu, Anti-Balaka.

Hali ya usalama inashindwa kudhibitiwa kwani vikosi vya kulinda amani kutoka Muungano wa Afrika havitoshelezi huku ghasia zinazofanywa sasa na wakristu nchini humo zikifananishwa na zile zilizochochewa dhidi ya jamii ya kiislamu huko Screbenica Bosnia Herzegovina mwaka 1995. Phillipe Leclerc ni mtaalamu wa ulinzi wa raia kutoka UNHCR na amekuwa akifanya kazi nchini humo kwa miezi miwili sasa na anasema maridhiano baina ya jamii tofauti Jamhuri ya Afrika ya Kati bado yawezekana lakini jamii ya kimataifa inatakiwa kusaidia serikali mpya kurejesha utawala wa kisheria.

(Sauti ya Leclerc)

“Mauaji kwa misingi ya kabila na dini yanaendelea magharibi na kaskazini mwa nchi yakilenga waislamu. Ni dhahiri watu wamenasa wakihaha kuokoa maisha yao. Haya yanaweza kuzuiwa kupitia maridhiano na uwepo wa jeshi la kimataifa. Si kwamba watu hawako tayari kukimbia, bali hawawezi. Usalama unatolewa na majeshi ya kimataifa iwe Ufaransa au askari 6,000 wa MISCA Lkini bado hawatoshi kulinda raia.

Muungano wa Afrika umepeleka askari 6,000 kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati ilhali Ufaransa imetuma askari 1,600.