ICC yaitaka DRC kuheshimu wajibu wake kwa mujibu wa mkataba wa Roma
Rais wa Baraza la nchi wanachama wa mkataba wa Roma unaounda mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC, Tiina Intelmann, ameitaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuheshimu mkataba wa Roma ambao nchi hiyo ni mwanachama.
Ametoa wito huo akizingatia kuwa Rais Omar Bashir wa Sudan yuko nchini humo kushiriki mkutano wa kikanda ihali ICC imempatia waranti mbili za kutaka akamatwe na afikishwe kwenye mahakama hiyo.
Bi. Intelmann amesema amemwandika barua waziri wa mambo ya nje wa DRC Raymond Tshibanda N'tungamulongo akimkumbusha wajibu wa serikali ya mwanachama wa mkataba wa Roma kutoa ushirikiano na mahakama hiyo.
Amesema baraza hilo mara kwa mara limerejelea wasiwasi wake juu ya madhara ya kushindwa kuzingatia uamuzi wa mahakama akishutumu vikali ziara ya watu wenye waranti za ICC kwenye nchi mwanachama wa mkataba wa Roma.
Amerejelea azimio namba 12/.3 la baraza hilo linalozuia mawasiliano na yeyote aliyepatiwa waranti na mahakama hiyo kwani kwa kufanya hivyo kunaathiri malengo ya mkataba wa Roma.