Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani kitendo cha gazeti moja Uganda kuweka hadharani majina ya wanaodaiwa kuwa mashoga

UM walaani kitendo cha gazeti moja Uganda kuweka hadharani majina ya wanaodaiwa kuwa mashoga

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani vikali kitendo cha gazeti moja nchini Uganda kuchapisha majina na picha za watu wanaodaiwa kuw ani mashoga na kusema kuwa kitendo hicho ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya faragha.

Msemaji wa Ofisi hiyo Cécile Pouilly amesema kitendo hicho kinadhihirisha hatari dhahiri dhidi ya kundi hilo baada ya kuridhiwa kwa sheria ya kupinga mapenzi ya jinsia moja na ushoga.

Amerejea hukumu ya awali ya mahakama ya juu kabisa nchini Uganda kuhusu kitendo cha gazeti la Rolling Stone kuchapisha orodha ya aina hiyo kuwa ni kinyume na haki za utu na faragha zilizowekwa bayana na katiba ya nchi hiyo.

Ofisi hiyo imerejelea wito wake kwa vyombo vya habari kujiepusha na uchochezi wa mashambulio ya chuki kwa misingi ya jinsi ya mtu huku ikitaka serikali kuchukua hatua za haraka kulinda watu wote dhidi ya ubaguzi au ghasia bila kujali jinsi au utambulisho wake.

Halikadhalika imetaka kupitiwa upya kwa vifungu vya sheria kuhusu uhalifu dhidi ya mashoga na waliobadili jinsi zao ili kuhakisha vitendo hivyo vinachunguzwa na wahusika wanafunguliwa mashtaka.