Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay alaani shambulio dhidi ya raia huko Yemen

Pillay alaani shambulio dhidi ya raia huko Yemen

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu Navi Pillay amelaani shambulio la leo lililofanywa na vikosi vya kijeshi vya Yemen bila ya uangalifu baada ya kukabiliwa na shambulio kusini mwa nchi hiyo.

Inaripotiwa kuwa kwenye tukio hilo jeshi la Yemen lilirusha makombora kwenye mji wa Al Dhale na kuua raia saba huku wanane wakijeruhiwa baada ya msafara wa kijeshi kushambuliwa.

Bi. Pillay katika taarifa yake ametaka kitendo cha kujibu mashambulizi bila kuchagua mahali au eneo la kupiga ni kinyume na haki za binadamu kwani  tangu mwezi Januari ofisi yake imepokea ripoti za matukio manane ya mashambulizi yakilenga hospitali, kliniki, shule na vyuo.

Amesema madai ya jeshi laYemenkuwa yalishambuliwa au ngome zake zilishambuliwa na watu waliokuwa wamejihami hayawezi kuhalalisha mashambulizi dhidi ya raia.

Kamishna huyo wa haki za binadamu amewakumbusha makamanda wa Jeshi la Yemeni kuwa wanawajibika kuhakikisha askari wao wanazingatia haki za kimataifa za binadamu hususan  haki ya kuishi hata pale wanapokabiliwa na wakati mgumu.

Amelitaka jeshi la serikali na vikundi vilivyojihaki kuhakikisha wanachukua hatua stahili kulinda raia dhidi ya mapigano ikiwemo kuepusha kulenga maeneo ya raia.