Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waonya kuendelea kuzorota kwa hali za wakimbizi wa ndani CAR

UM waonya kuendelea kuzorota kwa hali za wakimbizi wa ndani CAR

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ulio ziarani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati umejionea hali halisi na kuonya kuwa hali za wakimbizi wa ndani kwenye maeneo mbali mbali nchini humo zinazidi kuzorota na hatua za haraka zahitajika kusitisha mapigano na kuongeza usaidizi.

Valerie Amos ambaye ni Mkuu wa shirika umoja wa Mataifa linaloratibu usaidizi wa kibinadamu, OCHA pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS Michel Sidibé wamejionea kukata tamaa kwa wakazi wa nchi hiyo huko Bossangoa na mji mkuu Bangui.

Mathalani wakazi Elfu Hamsini wa mji wa Bossangoa wamekimbia makazi yao kukwepa mapigano kati ya wakristu na waislamu na walichoelezwa ni kwamba wakazi wamegawana upande wa mji huo kwa misingi ya kidini.

Umoja wa Mataifa unasema waislamu wamepata hifadhi kwenye shule ilhali wakristu wamehifadhiwa kwenye kanisa na kwamba hali ya mazingira ya kibinadamu kwenye makazi hayo ya muda inaweza kuwa mbaya siku za karibuni kutokana na matarajio ya kuanza kwa msimu wa mvua.

Bwana Sidibe baada ya kuzungumza na viongozi wa kidini wa pande zote ambao jitihada zao za kusitisha mapigano hayo zimegonga mwamba, ametaka machungu yanayokumba binadamu yakomeshwe. Anasema katika mapigano yanayoendelea hatma ya watoto na wanawake iko mashakani kutokana na ripoti za vitendo vya ubakaji na ukatili wa kingono mambo yanayoweza kusababisha maambukizi ya ukimwi.

Imam wa wilaya ya Boro huko Bossangoa, Ismaël Naffi ameeleza viongozi hao wa Umoja wa Mataifa kuwa wamechoshwa na vurugu na wanataka amani kwani hawataki kuondoka nchini mwao na kuelekea ukimbizini Chad.