Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na wadau wawezesha watoto milioni mbili katika migogoro kuendelea na masomo

UNICEF na wadau wawezesha watoto milioni mbili katika migogoro kuendelea na masomo

Japokuwa kumekuwa na madhara ya vita, maafa ya asili na dharura nyinginezo, takriban watoto milioni mbili katika nchi 20 kote duniani wamekuwa na uwezo wa kuendelea na masomo kwa kipindi cha miaka minne kutokana na ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na idara ya Tume ya Ulaya ya misaada ya kibinadamu na ulinzi wa raia.

Kamishna wa umoja wa Ulaya anayesimamia misaada ya kibinadamu, Christos Stylianides akizungumzia kwenye tukio hilo ameliambia Bunge la Ulaya kuwa wakati vita au migogoro mingine, watoto wanahitaji zaidi chakula, malazi na dawa.  Stylianides amesema kuwa elimu inaweza kuokoa maisha kwa kuwapa watoto nafasi ya usalama, kinga na kuhakikisha wanajifunza ujuzi kwa kujenga maisha yao ya baadaye na jamii zao na Umoja wa Ulaya unaongoza katika msaada wa elimu ya dharura.

Akizungumza wakati wa tukio hilo lililofanyika mjini Brussels ubelgiji baada ya kampeni ya mitandaoni ya miezi saba ya kuwahusisha na kulenga vijana katika nchi za ulaya kuelewa mpango wa elimu wakati wa dharura.  Kampeni hiyo kwa jina # masomo wakati wa dharurua iliwapasha habari na kuzieneza kupitia majukwaa tofauti na kusambazwa kwa karibu nchi 70 na kuwafikia watu zaidi ya millioni 70.

Katika kampeni hiyo watoto kutoka nchi mbali mbali kama vile Iraq, Ukraine, Nepal, na Guinea walisimulia hadithi zao za zamani ya kuendelea kujifunza licha ya vita, maafa ya asili na milipuko ya magonjwa.

Naibu mkurugenzi mkuu wa UNICEF Justin Forsyth amesema watoto wako tayari kwenda umbali wo wote ili kuendelea na elimu yao hata katika mazingira mabaya akiongezea kuwa jukumu kubwa ni kuhakikisha rasilimali muhimu zinapatikana.

Umoja wa Ulaya imeongeza msaada ya kibinadamu kwa asilimia 6% kwa mwaka wa 2017 na anatumaini wadau wengine watafanya hivyo. Kati ya watoto milioni 462 wenye umri wa shule na vijana wanaoishi katika nchi walioathirika wastani milioni 75 wanahitaji msaada wa elimu.

Msaada wa kampeni hiyo ulitoka kwa watu maarufu kutoka Uingereza, Italia, Slovenia, Slovakia na Hungary ikiwemo waigizaji filamu.