Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusishindwe kuwalinda wakimbizi wa ndani Sudan Kusini: Mtaalamu

Tusishindwe kuwalinda wakimbizi wa ndani Sudan Kusini: Mtaalamu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wakimbizi wa ndani, Chaloka Beyani amepaza sauti kwa Umoja huo na jamii ya kimataifa kupatia kipaumbele suala la ulinzi na usalama wa wakimbizi wa ndani Sudan Kusini.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu imemkariri Beyani akisema kuwa mapigano nchini humo yamesababisha wengi kupoteza makazi na kuzorota kwa hali ya usalama na ghasia zinaendelea licha ya makubaliano ya kumaliza uhasama yaliyofikiwa tarehe 23 mwezi huu wa Januari.

Amesema katika kushughulikia hali hiyo, kipaumbele lazima kielekezwe kwenye usalama na kuepuka kabisa kushindwa kuwapatia ulinzi wananchi waliopoteza makazi akigusia mashambulizi yanayolenga raia wakiwemo wanawake na watoto akisema kuwa hayakubaliki.

Bwana Beyani alitembelea Sudan Kusini mwezi Novemba mwaka jana mojawapo ya mapendekezo yake ni kuweka mfumo mmoja wa kulinda wakimbizi wa ndani.

Mapigano Sudan Kusini  yaliyoanza tarehe 15 Disemba 2013 yamesababisha watu wapatao 700,000 kupoteza makazi yao.