Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi maalumu wazinduliwa kuzuia tatizo la kudumaa Malawi:WFP

Mradi maalumu wazinduliwa kuzuia tatizo la kudumaa Malawi:WFP

Mradi mpya wenye nia ya kupambana na tatizo la kudumaa umezinduliwa leo Jumatano nchini Malawi limesema shirika la mpango wa chakula duniani WFP. Kutokuwepo kwa usalama wa chakula mara kwa mara, lishe duni na kujirudia kwa maradhi ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha kudumaa, miongoni mwa karibu watoto milioni moja wa Malawi walio chini ya umri wa miaka mitano , ambao ni nusu ya watoto wote wa umri huo nchini humo.

Mradi huo unaotekelezwa kwenye wilaya ya Ntchisi jimbo la Kati utawafikia kina mama na watoto 600,000 katika miaka mitatu na nusu ijayo. Lengo lake ni kupunguza tatizo la kudumaa kwa asilimi 5 hadi 10 na kujenga uwezo wa kupambana na tatizo hilo.

Mradi huo umezinduliwa Malawiambayo ni moja ya nchi zenye viwango vikubwa vya kudumaa duniani na baadaye utazinduliwa Msumbiji. Mradi huo umefadhiliwa na fuko la uwekezaji kwa watoto CIFF, na unaungwa mkono na serikali ya Malawi, WFP, mpango wa kuchagiza lishe SUN na mshirika wa WFP World Vision.