Silaha za Kemikali Syria ni ukumbusho wa haja ya kuzitokomeza: Ban

21 Januari 2014

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa kamati kuhusu utokomezaji wa silaha kufanya juhudi ili kuondoa mkwamo uliopo kwa mpango wake wa kuchukua hatua.

Bwana Ban amesema matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria yalikuwa ukumbusho wa haja ya kukabiliana na hatari zinazoletwa na silaha zote za mauaji ya halaiki, zikiwemo silaha za nyuklia.

Akihutubia kikao cha ufunguzi wa kamati hiyo ya kutokomeza silaha mjini Geneva leo, Bwana Ban ameutaja mkataba kuhusu silaha za kemikali kama ufanisi wa kuaziziwa wa kamati hiyo, na kutoa wito kwa nchi wanachama kuzing’oa tofauti zao ili zisaidie kujena ulimwengu ulo salama zaidi

 “Ni lazima tukabiliane na hali halisi ya karne ya 21. Kamati kuhusu utokomezaji silaha inaweza kuto msukumo wa kuwa na dunia salama zaidi na mustakhbali bora. Hilo ndilo jukumu lake. Kama mjuavyo nyote, nimeweka utokomezaji silaha na kukomesha uzagaaji wa silaha kama jambo la kipaumbele kwenye ajenda ya Umoja wa Mataifa. Chombo kinachofanya kazi kinaweza na ni lazima kichangie kwa kiasi kikubwa amani na usalama wa kimataifa. Fedha zinazookolewa kutokana na kutokomeza silaha zinaweza kuchangia maendeleo na maisha bora kimataifa. Kazi yenu inaweza kuleta mabadiliko makubwa, wakati jamii ya kimataifa inapojitahidi kufikia malengo ya maendeleo ya millennia na kubuni ajenda thabiti ya maendeleo baada ya mwaka 2015.”

Kamati ya utokomezaji silaha iliundwa mnamo mwaka 1979 kama ukumbi wa kujadili udhibiti wa silaha na mikataba ya uondoaji silaha.