Waathirika wa kimbunga nchini Ufilipino bado wanahitaji misaada.

16 Januari 2014

Miezi miwili baada ya kimbunga Typhoon Haiyan kuikumba Ufilipino hatua kubwa zimechukuliwa katika maeneo mengi katika kujikwamua baada ya janga hilo la asili lakini bado watu wanategemea misaada ya kiutu hususani katika kujenga upya makazi yao, amesema mkuu wa shirika la kuratibu misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa OCHA Valerie Amos

Bi Amos amesema katikati ya mwezi December alizindua uchangiaji wa zaidi ya dola milioni mia saba kutoa msaada kwa waathirika milioni tatu na wengine milioni saba lakini anasikitishwa kwamba ni asilimia 20 pekee ya fedha hizo zimetumika kununulia vifaa kwa ajili ya ujenzi upya wa nyumba za walioathirika.

Amesema wakati huu ambapo msimu wa mvua umekaribia na mvu za awali zimeanza kusababaisha ukosaji wa makazi, msaada wa dharura unahitajika kwa ajili ya zana na mbegu ili wakulima wawe tayari kwa ajili ya msimu ujao wa kuotesha.

 Mkuu huyo wa OCHA ameongeza kuwa wahisani, mashirika ya kiutu na watu wa Ufilipino wamechangia kiwango kikubwa lakini ufikishaji wa misaada kwa walengwa umekumbwa na sintofahamu. Pia amesema huduma ya umeme siyo ya uhakika katika sehemu kubwa ambazo zilikumbwa na kimbunga Typhoon Haiyan huku pia shule zikikumbwa na mkwamo kufuatia ukosefu wa maeneo ya kujifunzia na vifaa licha ya kufunguliwa January 6 mwaka huu.

Hata hivyo amesema katika miezi michache ijayo jamii ya misaada ya kiutu itaondokana na mpango wa misaada ya dharura na kujikita katika mpango wa muda mrefu wa misaada na juhudi za ujenzi upya  na kwamba mkakati  huu unatagemea usaidizi zaidi wa wahisani.

Zaidi ya watu milioni 14 walikumbwa na kimbunga hicho ambapo miongoni mwao watu milioni nne na laki moja walipoteza makazi kufuatia kadhia hiyo.