Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ziarani Ufilipino, Ban ahuzunishwa na uharibifu wa kimbunga Haiyan

Ziarani Ufilipino, Ban ahuzunishwa na uharibifu wa kimbunga Haiyan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, ambaye yupo ziarani nchini Ufilipino, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Benigno Simeon C. Aquino III wa Ufilipino, wakiangazia hasa juhudi za kibinadamu na kujikwamua kwa taifa hilo kufuatia janga la kimbunga Haiyan (Yolanda).

Bwana Ban amepongeza ushirikiano bora baina ya serikali ya Ufilipino, mashirika ya kibinadamu na Umoja wa Mataifa katika utoaji huduma za kibinadamu na juhudi za kujikwamua, na kuongeza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia mikakati hiyo inayoongozwa na serikali ya Ufilipino. Baadaye, Bwana Ban amekutana na waandishi wa habari, na kuelezea masikitiko yake

“Nimehuzunishwa sana na kufadhaishwa na kile nilichoona. Vifo vingi na uharibifu ulokithiri. Ni vigumu kuelezea. Naweza vipi kuelezea ninavyohisi baada ya kuona majanga na taabu mliyomo sasa? Nawapa pole za dhati kwa yale mliyopitia- kuwapoteza wapendwa, watu wengi kujeruhiwa na uharibifu huu wa jamii yenu. Kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, nipo hapa kuonyesha mshikamano wangu thabiti na ule wa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa.”

Amesema kimbunga Haiyan ni mfano wa jinsi matukio yatokanayo na hali mbaya ya hewa yanavyoathiri maisha ya watu, na hivyo kusisitiza haja ya kujiandaa na kupunguza athari hizo.