Suala la jinsia bado lina umuhimu kwenye usajili wa watoto: UNICEF

11 Disemba 2013

Suala la jinsia limeelezwa kuwa na umuhimu mkubwa kwenye usajili wa watoto pindi wanapozaliwa kwani katika nchi nyingi uwepo wa baba unarahisisha mtoto kusajiliwa na kupata cheti. Mtakwimu kutoka shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Claudia Cappa amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini New York, kuhusu ripoti ya shirika hilo inayoangazia usajili wa watoto wanaozaliwa na mwelekeo duniani kote.

Amesema ijapokuwa hakuna tofauti katika usajili wa watoto wa kike na wa kiume pindi wanapozaliwa, lakini mtoto anayezaliwa katika familia ya mama pekee anakumbwa na mazingira magumu katika kusajiliwa.

 (Sauti ya Claudia)

 Wanawake wanaolea watoto peke yao mathalani,katika baadhi ya nchi hawaruhusiwi kusajili watoto wao. sambamba na hilo suala kwamba utaifa wa mtoto ambao wakati mwingine unategemea utaifa wa baba. Kwa hiyo jinsia inahusika, lakini linapokuja suala la usajili kwa ujumla hatukuona tofauti."

Naye Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Geeta Gupta Rao akiangazia zaidi ripoti hiyo amesema kwa kiasi kikubwa mifumo ya usajili wa raia ikiwemo ile ya vizazi bado ni dhaifu kwenye nchi nyingi duniani. Amesema UNICEF ili kupata takwimu hizo, inategemea zaidi takwimu zinazochukuliwa katika kaya na zile za kidemografia.