Utashi wa kisiasa ni muhimu ili kulinda haki za binadamu: Ban

9 Disemba 2013

Kufikia usimamizi stahili wa haki za binadamu ulimwenguni kumesalia kwenye utashi wa kisiasa wa viongozi wa nchi husika, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon katika ujumbe wake wa kuelekea kuadhimisha siku ya haki za binadamu tarehe 10 Disemba.

Bwana Ban amesema miaka Sitini na Mitano tangu kupitishwa kwa tamko la kimataifa la haki za binadamu na miongo miwili baada ya kuanzishwa kwa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa jitihada zimeendelea kutetea wanyonge, kushinikiza serikali kuwajibika na kuunga mkono watetezi wa haki, lakini bado utashi wa kisiasa unahitajika.

Amesema serikali ndio zina wajibu wa kwanza katika ngazi ya kitaifa kulinda raia na kuepusha ukiukwaji haki na pia kupaza sauti iwapo nchi jirani inashindwa kutekeleza wajibu wake.

Bwana Ban amesema jambo hilo si rahisi mara nyingi kwani katika miaka 20 iliyopita, dunia imeshuhudia mauaji ya kimbari na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa.

Amesema kwa sasa juhudi zinaendelea kuimarisha mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia majanga yanayoibuka na kuzuia ukiukwaji haki, lakini ametaka nchi nazo kutekeleza ahadi zao za mkutano wa Vienna.