Wakati misaada inaendelea kuwasili Ufilipino kuwafikia walengwa bado ni changamoto:

13 Novemba 2013

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, kimataifa na wadau wengine wanaendelea kupeleka watu na misaada nchini Ufilipino lakini kuwafikia walengwa bado ni changamoto, kwani miundombinu imeharibika vibaya na mawasiliano ni shida. Flora Nducha na taarifa kamili

(RIPOTI YA FLORA NDUCHA)

Timu ya shirika la afya duniani WHO na wahudumu wengine wamewekwa tayari kupelekwa kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi na kimbunga Haiyan, huku madawa na vifaa vingine vikiwasili kwenye mji wa Cebu vikisubiri kupelekwa vinakohitajika zaidi ikiwemo mji uliosambaratika kabisa wa Tacloban.

WHO inashirikiana na serikali ya Ufilipino kupeleka timu za kimataifa kutathimini na kusaidia hali halisi , hadi sasa timu ya watu tisa kutoka Australia, Belgium, Germany, Hungary, Japan, New Zealand, Switzerland ana Marekani wamethibitisha wako njiani au wameshawasili Ufilipino.

Hata hivyo mawasiliano ni tatizo kubwa na ndio maana muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU umepelekwa vifaa vya mawasiliano vya satellite ili kurejesha mawasiliano nchini humo ambayo ni muhimu saana kwa ajili kutatufa manusura na shughuli za uokozi. ITU inasema kufuathia athari za kimbunga hicho itachukua wiki kadhaa au miezi kukarabati miundombinu ya mawasiliano nchini Ufilipino.