Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuimarishe usimamizi wa maliasili kwenye maeneo ya mizozo: Ban

Tuimarishe usimamizi wa maliasili kwenye maeneo ya mizozo: Ban

Ulimwenguni kwa kiasi kikubwa kumesheheni taarifa juu ya umuhimu wa mazingira kwa maendeleo endelevu lakini wakati huo huo kiwango cha utumiaji hovyo wa maliasili kama vile misitu, wanyamapori, vyanzo vya maji na hata ardhi ya kilimo kinazidi kuongezeka.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kwenye salamu zake maalum kwa siku ya kimataifa ya kuzuia uharibifu wa mazingira kwenye maeneo ya vita na mizozo.

Bwana Ban ametolea mfano Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako amesema usafirishaji haramu wa madini, wanyamapori, magogo, mkaa pamoja na dawa za kulevya vinasaidia vikundi vyenye silaha na mitandao ya wahalifu, Huko Somalia amesema yakadiriwa biashara haramu ya mkaa yapatia vikundi vya kigaidi na waasi mapato ya dola Milioni 384.

Katibu Mkuu ametaka siku ya leo kutumiwa vyema na nchi wanachama kuimarisha usimamizi bora wa maliasili hususan kwenye maeneo yenye mizozo ili kuzuia uwezekano wa mapato yatokanayo na biashara haramu kuzidi kuchochea migongano.