Maonyesho ya nchi za Kusini yaanza Nairobi:

28 Oktoba 2013

Maonyesho ya wiki moja ya miradi na mbinu za maendeleo zinazojali mazingira yameanza mjini Nairobi, Kenya yakihusisha nchi zinazoendelea. Maonyesho hayo yameandaliwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia ushirikiano wa nchi zinazoendelea, SOUTH-SOUTH yanafanyika wakati huu ambapo uchumi wa nchi hizo unachangia asilimia 47 kwenye biashara ya dunia. Ripoti ya Alice Kariuki inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Alice)

Maonyesho hayo yakienda sambamba na mijadala ya wajumbe zaidi ya 150 kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa na nchi zinazoendelea yanalenga kubadilishana na kuibua mbinu bunifu na za ushirikiano baina ya nchi hizo na hivyo kubadili mwelekeo uliozoeleka kwa ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea na zile tajiri.

Mathalani miradi ambayo tayari ina manufaa kwa mazingira, uchumi na hata kutoa fursa za ajira.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson akizungumza kwenye ufunguzi amesema nchi zinazoendelea zina mambo mengi ya kushirikiana kuliko tofauti na hivyo ushirikiano baina yao ndio suluhu ya stahili ya changamoto zinazowapata.

(Sauti ya Eliasson)

Wenyeji wa maonyesho hayo ni shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, UNEP ambalo Mkurugenzi wake Mkuu Achim Steiner amesema uchumi unaojali mazingira una manufaa na hakuna nchi inayoweza kufanikisha bila ushirikiano.

(Sauti ya Steiner)

Katika maonyesho hayo wataalau watawasilisha mpango wa nishati wa nchi za Kusini, mpango ambao unatoa fursa ya kujadili kwa pamoja masuala yanayoibuka kwenye sekta ya nishati.