Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twapongeza jitihada za AU za kuleta maridhiano Sudan na Sudan Kusini: Eliasson

Twapongeza jitihada za AU za kuleta maridhiano Sudan na Sudan Kusini: Eliasson

Mashauriano ya pili ya ngazi ya mawaziri kutoka Sudan na Sudan Kusini yamefanyika hii leo mjini New York, mada kuu ikiwa ni mchakato wa amani wa kumaliza mzozo kati ya nchi mbili hizo. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaidi.

 (Taarifa ya Assumpta)

Sudan na Sudan Kusini ziliwakilishwa na mawaziri wao wa mambo ya nje ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Elisson alieleza kuwa hofu inayokumba umoja huo kutokana na machungu yanayoendelea kuwapata wananchi wa nchi hizo. Mathalani utapiamlo, mapigano na ukosefu wa huduma muhimu za kibinadamu hususan kwenye maeneo ya migogoro kama vile Kordofan Kusini na Darfur hukoSudanna jimbo la Jonglei Sudan Kusini bila kusahau huko Abyei. Amepongeza juhudi za Umoja wa Afrika za kuleta amani akisema kuwa Umoja wa Mataifa uko pamoja nao kwenye harakati hizo, hata hivyo…

 (Sauti ya Eliasson)

"Mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili Sudan na Sudan Kusini zifikie uhusiano mzuri na ushirikiano katika masuala yote. Ni muhimu kumulika masuala yaliopo sasa ya mipaka ili kuepukana na uhasama, kuimarisha kuaminiana  na kuweka amani ya kudumu.Naomba serikali zote kutatua  suala lililokwama kuhusu Abyei na kuweka mikakati ya usalama mipakani ili kuzuia mizozo"

 Katika kikao hicho pande mbili zilionesha wasiwasi kuhusu masuala ya usalama hususan mpaka mahsusi wa eneo lisilopaswa kufanyika shughuli za kijeshi na tuhuma za kila upande kusaidia waasi. Thabo Mbeki kutoka jopo la ngazi ya juu la Umoja wa Afrika ambao wanaratibu mazungumzo hayo akafafanua..

 (Sauti ya Mbeki)

 “Kwa haya mambo mawili kuhusiana na usalama, yanashughulikiwa na nchi mbili hizo na nafikiri yakiwa na matarajio chanya.”