Rasimu ya azimio kuhusu Syria yawasilishwa Baraza la Usalama, kupigiwa kura: Balozi Churkin

27 Septemba 2013

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Alhamisi limekuwa na mashauriano ya faragha kuhusu Syria ambapo Urusi na Marekani ziliwasilisha rasimu ya azimio kwa Syria, kufuatia shambulio la kemikali kwenye eneo la Ghouta, nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus,tarehe 21 mwezi uliopita. Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Vitaly I. Churkin amewaeleza waandishi wa habari kuwa rasimu hiyo inafuatia mazungumzo ya hivi karibuni katika mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Urusi na kwamba wana Imani rasimu hiyo itapitishwa penginepo kesho jioni kuwa azimio. Amesema rasimu imeweka bayana mambo ya msingi ikiwemo kujumuisha kwa mara ya kwanza katika viambatanisho makubaliano ya Geneva kuhusu Syria yaliyopitishwa mwaka jana. Balozi Churkin amesema kitendo hicho kinapatia nguvu makubaliano hayo. Akizungumzia rasimu hiyo, Mwakilishi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Marl Lyall Grant amesema ni la aina yake na limegusia masuala ya silaha za kemikali, taratibu za kutoa ripoti na hatua za kuchukuliwa iwapo pande yoyote nchini Syria itakiuka pamoja na upatiaji suluhu la kisiasa mzozo wa Syria. Balozi Grant amesema rasimu hiyo kwa mara ya kwanza inaonyesha umoja ndani ya baraza juu ya Syria hususan kwenye matumizi ya silaha za kemikali.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter