Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada za kulinda watu zaendelea kukumbwa na changamoto: Ban

Jitihada za kulinda watu zaendelea kukumbwa na changamoto: Ban

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limefanya mashauriano kuhusu Wajibu wa kulinda ikiangazia zaidi nafasi ya serikali kulinda raia wake dhidi ya majanga na kuzuia majanga hayo kutokea ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema jitihada hizo bado zinakumbana na changamoto. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Mauaji yanaendelea na jitihaza za kuyazuia zinazidi kukumbwa na vikwazo, Ni Bwana Ban wakati akizungumza na washiriki wa mashauriano hayo akisema kuwa mzozo wa Syria ni mfano dhahiri. Amesema ripoti yake kwenye mkutano huo inaeleza bayana kuwa kushindwa kwa jitihada za pamoja kuzuia mzozo huo miaka miwili na nusu iliyopita, kutabakia kuwa mzigo mkubwa kwa msimamo wa Umoja wa Mataifa na nchi wanachama. Hata hivyo amesema anatarajia kuwa mazungumzo kuhusu uhifahi wa silaha za kemikali za Syria yatawezesha baraza la usalama kumaliza janga la Syria, lakini akakumbusha kuwa serikali zina wajibu wa kulinda raia dhidi ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita, mapigano ya kikabila, lakini wajibu huo haupaswi kusubiri hadi hali inapokuwa mbaya, bali anasema..

(SAUTI YA BAN)

“Lakini hebu pia tukumbuke wajibu wa kulinda haulengi kulinda raia wakati mambo yameshaharibika, la hasha! Kwanza kabisa lengo ni kuzuia majanga yasitokee kabisa. Hii ndio lengo kuu la ripoti yangu mpya: kulinda kwa kuzuia. Kuzuia kunaweza kuonekana ni jambo la kufikirika lakini ni jambo thabiti na mahsusi.”