Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

INTOSAI sasa kukagua utekelezaji wa mikataba ya kuhifadhi mazingira

INTOSAI sasa kukagua utekelezaji wa mikataba ya kuhifadhi mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mazingira UNEP limetiliana saini na chombo cha kimataifa cha ukaguzi, INTOSAI kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa mikataba 280 inayohusu mazingira ambayo ilisainiwa katika siku zilizopita.

Mikataba hiyo ni pamoja na ile inayohusu mabadiliko ya tabia nchi,taka hatarishi na maeneo mengine yanyohusu dunia kwa ujumla.

Makubaliano hayo ambayo yamesainiwa katika ofisi za UNEP mjini Nairobi ni sehemu ya mpango wa kumulika maendeleo yanayopigwa juu ya ufikiaji wa malengo ya maendeleo ya milenia. Akizungumza baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Mkuu wa UNEP Achim Steiner amesema kuboresha ufuatiliaji na tathmini ya hatua za serikali na makundi mbali mbali katika kutekeleza mikataba ni muhimu katika kufikia malenyo ya kimataifa yaliyowekwa ili kupata maendeleo endelevu kwa wote.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na UNEP ilibaini kuwepo kwa usimamizi hafifu wa utekelezaji wa mikataba ya kimataifa inayohusu mazingira.