Bado nasisitiza suluhisho la kisiasa kwa mgogoro wa Syria: Ban

4 Septemba 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ambaye yuko ziarani barani Ulaya, ametoa mhadhara kwenye Chuo Kikuu cha St. Petersburg nchini Urusi na kusema kuwa yeye bado anaendelea kusisitiza suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria. Ripoti ya Assumpta Massoi inafafanua zaid.

(Ripoti ya Assumpta)

Mhadhara wa Katibu Mkuu kwa wanafunzi wa chuo hicho kikuu uligusia masuala kadhaa ikiwemo malengo ya maendeleo ya milenia, ukosefu wa ajira, uchumi, madhila ya kijamii na kile kinachoendelea hivi sasa nchini Syria. Bwana Ban amesema wakati huu si wa kutafuta suluhu ya zimamoto, bali ni lazima dunia ijikite kujenga msingi wa kupatia suluhu la kudumu mzozo huo. Amerejelea tena kuwa iwapo ikibinainika silaha za kemikali zilitumika Syria, basi itakuwa ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu. Lakini kubwa zaidi pande zinazopingana ziweke silaha chini na kuanza mazungumzo.

(Sauti ya Ban)

“Naendelea kushinikiza suluhu ya kisiasa. Upelekaji silaha na nguvu za kijeshi vyazidi kuendeleza umwagaji damu. Ni wakati wa pande pinzani kuacha mapigano na kuanza mazungumzo. Wananchi wa Syria wanahitaji amani. Naamini kwa dhati tuna wajibu wa kushughulikia haraka migogoro katika dunia yetu. Na wakati huo huo tunapaswa kuangalia kwa mapana zaidi na kwa muda mrefu na kuchukua hatua kukabiliana na changamoto za muda mrefu.”