Kay akaribisha mkataba wa Juba uliosainiwa Addis Ababa:

28 Agosti 2013

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia na mkuu wa UNSOM bwana Nicholas Kay leo amekaribisha mkataba uliotiwa saini mjini Addis Ababa kati ya waziri wa nchi Farah Sheikh Abdulkadir na Sheikh Ahmed Mohamed Islaan “Madobe”kwa niaba ya serikali ya mpito na utawala wa muda wa Jubba .

Nayo Ethiopia ikiwa ni mwenyekiti wa IGAD imeweka sahihi yake kama mdhamini. Muafaka huo unaanzisha mkakati wa uongozi na utawala katika eneo la Lower Juba, Juba ya Kati na Gedo katika kipindi kijacho.

Bwana Kay amesema hii ni hatua muhimu katika kuelekea kurejesha amani Somalia, kuwa na serikali imara ya shirikisho ya Somalia na kuchangia katika usalama wa kikanda na kimataifa, kwani makubaliano hayo yanafungua mlango wa mustakhbali mzuri kwa Somalia.

Bwana Kay pia amempongeza Ahmed Madobe kwa kuwa kiongozi wa mpito wa Jubba. Amesema pande zote zitafaidika na muafaka huo na amezitaka kutekeleza makubaliano kwa dhati.