Seoul watoa maoni juu ya haki za binadamu DPRK, baadaye ni Tokyo

Seoul watoa maoni juu ya haki za binadamu DPRK, baadaye ni Tokyo

Maoni ya umma kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Korea Kaskazini  yataanza kutolewa huko Tokyo, Japan wiki ijayo mbele ya jopo la Umoja wa Mataifa lililoundwa kuchunguza vitendo hivyo. Jopo hilo litafanya kazi kwa siku mbili ambapo maoni yanayokusanywa ni pamoja na DPRK kuteka nyara raia wa Japani. Kwa sasa jopo hilo liko Korea Kusini kwa siku tano hadi Jumanne ijayo litakapoelekea Tokyo na kwa sasa linasikiliza maoni ya umma na kufanya mashauriano juu ya masuala ya haki za binadamu. Masuala hayo ni pamoja na kambi za kisiasa, utesaji na mauaji ya watu kwa misingi ya imani ya kidini na haki ya chakula. Wanaotoa shuhuda ni pamoja na mashahidi ambao hivi karibuni walitoroka Korea Kaskazini. Michael Kirby ambaye ni Mwenyekiti wa jopo hilo la watu watatu amesema ukusanyaji wa maoni ya umma huko Seol na Tokyo ni mojawapo ya njia ya kuhabarisha umma juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu Korea Kaskazini, kwa kuwa hadi sasa jopo hilo halijaruhusiwa kuingia nchini humo kupata picha halisi na hata jitihada za kualika serikali ya DPRK kwenye vikao vyake hazikuzaa matunda. Ripoti ya jopohiloitawasilishwa kwenye baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Oktoba mwaka huu.