Naibu Katibu Mkuu azungumzia silaha za kemikali Syria, UNICEF yalaani

22 Agosti 2013

Suala la Syria limechukua sura mpya baada ya kuwepo kwa ripoti za matumizi ya silaha za kemikali siku ya Jumatano ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amezungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu na kusema kitendo hicho kina madhara makubwa kwa binadamu. Taarifa ya Alice Kariuki inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Alice Kariuki)

Bwana Eliasson amesema ni matumaini kuwa jopo la Umoja wa Mataifa linaloongozwa na Profesa Ake Sellstrom huko Syria litaweza kupata fursa ya kufika eneo hilo kwa ridhaa ya serikali ya Syria.

(Sauti ya Eliasson)

“Kile ambacho tukio hilo limeonyesha ni kwamba ni lazima tudhibiti huu mgogoro. Tayari tumeona athari zake kikanda na sasa uwezekano wa matumizi ya silaha za kemikali ambalo ni lazima lichunguzwe. Nisema tu kwamba hakuna uthibitisho. Tunawasiliana na serikali ya Syria ni matumaini yetu kuwa pande zote zitatoa ushirikiano ili tuweze kufanya uchunguzi. Pia twatumai kuwa kila mtu atatambua umuhimu wa kumaliza uhasama.”

Wakati huohuo shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema watoto ni lazima walindwe , baada ya ripoti kwamba silaha za kemikali zimetumika kwenye machafuko yanayoendelea nchini Syria ambayo yameshasababisha vifo vingi vikiwemo vya watoto.

Kwa mujibu wa UNICEF mashambulizi dhidi ya raia wakiwemo watoto yaliyofanyika nje kidogo ya Damascus yanasikitisha na kitendo hicho cha kikatili ni lazima kiwe kumbusho kwa pande zote zenye ushawishi katika vita hivyo kwamba machafuko yamefurutu ada na watoto wameteseka vya kutosha.