Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa umeazimia kupatia suluhu mzozo DRC: Kobler

Umoja wa Mataifa umeazimia kupatia suluhu mzozo DRC: Kobler

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC Martin Kobler amehitimisha ziara yake ya siku tatu huko Kivu Kaskazini na kusisitia azma ya Umoja huo katika kusaidia kurejesha mamlaka mashariki mwa nchi hiyo, amani na utulivu. Amegusia vikundi vyenye silaha huko Kivu Kaskazini na Kusini na maeneo mengine ya Mashariki mwa DRC ambako mapigano yamesababisha raia kukimbia.

Akiwa Goma, Bwana Kobler ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo mwezi Juni, alikuwa na mazungumzo na mamlaka za eneo hilo pamoja na vikosi vya usalama na watendaji wa Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa ajenda katika mazungumzo yao ni matarajio ya MONUSCO na brigedi ya Umoja wa Mataifa ya Kujibu mashambulizi iwapo kutakuwepo na mashambulio dhidi ya raia huko Kaskazini Kivu.