Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washauri wa UM wahofia hali nchini Misri

Washauri wa UM wahofia hali nchini Misri

Washauri wiwili maalum wa Umoja wa Mataifa wameelezea wasiwasi wao kuhusu machafuko yalotekelezwa Jumatano asubuhi nchini Misri, ambako vikosi vya usalama vimedaiwa kutumia nguvu zilokithiri dhidi ya waandamanaji mjini Cairo.

Adama Dieng ambaye ni mshauri kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari na Jennifer Welch, ambaye ni mshauri kuhusu wajibu wa kulinda, wamesema ingawa idadi kamili ya wahanga na majeruhi haijathibitishwa, wamesikitishwa na idadi kubwa ya vifo na kuongezeka kwa machafuko nchini humo.

Wameelezea kushtushwa hasa na kulengwa kwa makanisa ya Wakristo na taasisi kadhaa, zikiwemo katika mikoa ya Assiut, Fayoum, Minya na Sohag kwa madai ya kulipiza kisasi kufuatia matukio mjini Cairo.

Wametoa wito kwa raia wote wa Misri kuwajibika katika vitendo vyao wakati huu mgumu, na kujiepusha na ghasia kama njia ya kuelezea kero zao, hususan kwa kulenga watu wa dini tofauti na taasisi zao, au lugha na vitendo ambavyo vitaifanya hali kuzorota zaidi.