Pillay ataka hatua za dharura kuepusha janga zaidi nchini Misri

15 Agosti 2013

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu Navi Pillay amezisihi pande zote nchini Misri kujizuia kutumbukia kwenye janga zaidi baada ya siku moja ya umwagaji damu nchini humo Jumatano ambayo imesababisha vifo vya mamia ya watu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Nalaani vikali vifo vya watu nchini Misri na nataka pande zote nchini humo kutafuta njia ya kuondokana na ghasia hiyo na serikali na vikosi vya usalama vijizuie zaidi, ni kauli ya Kamishna Mkuu Pillay.

Amesema kumekuwepo na ripoti mkanganyiko juu ya wigo wa ghasia za Jumatano pindi vikosi vya usalama vilipoingia kuondoa waandamanaji waliokuwa wamekusanyika kwa siku kadhaa mjini Cairo. Taarifa za serikali zilieleza kuwa waliokufa ni zaidi ya Mia Tano ilhali chama cha Udugu wa kiislamu, kilitangaza idadi kuwa ni zaidi ya Elfu Mbili.

Bi. Pillay amesema hata idadi inayotolewa na serikali inadhihirisha matumizi ya kupita kiasi ya nguvu dhidi ya waandamanaji na hivyo kunapaswa kufanyika kwa uchunguzi huru juu ya vitendo vya vikosi vya usalama na yeyote atakayethibitika kuwa alivunja sheria, awajibishwe.