Benki ya dunia yaidhinisha mradi wa umeme kwenye maporomoko ya mto Rusumo

7 Agosti 2013

Benki ya dunia kupitia bodi yake ya utendaji imeidhinisha dola Milioni 340 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia nguvu za maji kwenye maporomoko ya mto Rusumo ulioko ukanda wa maziwa makuu barani Afrika.Mradi huo unalenga kunufaisha wakazi Milioni 62 walioko Burundi, Rwanda na Tanzania na unafuatia ziara ya Rais wa Benki ya dunia Jim Yong Kim na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwenye ukanda huo mwezi Mei mwaka huu.

Colin Bruce ambaye ni Mkurugenzi wa mikakati na operesheni kwenye Benki ya dunia amesema kukamilika kwa mradi huo kutatoa hakikisho la upatikanaji wa umeme, kutapunguza gharama za umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi zitakazowezesha kuongeza upatikanaji wa ajira.

Amesema uhaba wa umeme kwenye eneo hilo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ambapo ni asilimia nne tu ya wananchi wa Burundi wanapata huduma ya umeme ilhali Rwanda ni asilimia 13 na Tanzania ni asilimia 15.