Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili ushirikiano baina ya UM na jumuiya za kikanda

Baraza la Usalama lajadili ushirikiano baina ya UM na jumuiya za kikanda

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadilia suala la ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda. Kikao cha leo kimesimamiwa na rais wa Argentina Christina Fernández de Kirchner, na kuhutubiwa na Katibu Mkuu Ban Ki-Moon. Joshua Mmali ana maelezo zaidi

(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Jumuiya na mashirika ya kikanda yana ufahamu mkubwa, ujuzi na mitandao ya kikanda ambavyo vyote ni muhimu katika upatanishi, kuandaa mipango ya operesheni za ulinzi wa amani na kujenga amani ya kudumu. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, wakati wa kikao cha leo cha Baraza la Usalama kuhusu ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda.

Bwana Ban amesema licha ya changamoto nyingi zinazojitokeza wakati wa ushirikiano huo, ana imani thabiti katika thamani ya kuunganisha nguvu za kila ukanda.

"Jumuiya nyingi za kikanda zina historia ndefu ya kuhusika katika kuzuia mizozo na upatanishi, ulinzi wa amani na ujenzi wa amani. Mengine yameanza kujikita katika Nyanja hizi. Kama Katibu Mkuu, nimejionea mwenyewe thamani ya ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda kote duniani. Ni kupitia katika ushirikiano tu ndipo tutaweza kufikia ndoto zetu za dunia yenye amani zaidi."

Katika hotuba yake, rais wa Argentina Christina Fernández de Kirchner, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kama huo.

"Katika miaka ya hivi karibuni, jumuiya mpya na mashirika ya kikanda yamechangia pakubwa katika kuzuia mizozo na katika kuendeleza na kudumisha amani na usalama wa kimataifa.Jumuiya zingine zimeongeza uwezo wao wa kuchukua hatua katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kama inavyoonekana katika operesheni kadhaa za kulinda amani."