Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jitihada zifanyike yaliyotokea Hiroshima na Nagasaki yasitokee tena

Jitihada zifanyike yaliyotokea Hiroshima na Nagasaki yasitokee tena

Mkutano wa kimataifa wa kuzuia kuenea kwa silaha duniani umefanyika hii leo huko Geneva, Uswisi ambapo pamoja na kujadili uundwaji wa kikundi cha kuandaa mpango kazi, umekumbuka madhila ya mashambulio ya mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki nchini Japan miaka Sitini na Minane iliyopita na kutaka mashambulio ya aina hiyo yasitokee tena.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mwakilishi wa Japani kwenye mkutano huo Balozi Mari Amano amesema huko Hiroshima kumefanyika kumbukumbu na Nagasaki itafanyika Alhamisi ambapo amekumbusha kuwa azma ya wananchi wa Japani ya kutokomeza silaha za nyuklia haijabadilika tangu mwaka 1945.

(SAUTI YA AMANO)

"Naamini hilo ni lengo ambalo linaungwa mkono na jamii nzima ya kimataifa ikiwemo sote ndani ya chumba hiki cha baraza. Ijapokuwa idadi ya silaha za nyuklia duniani inapungua bado Japani haijaridhika hususan kwa kuzingatia kwamba tunafahamu madhara yaliyosababishwa na mlipuko mmoja tu wa bomu la atomiki. Katika mkutano uliofanyika wiki iliyopita huko Hiroshima, Waziri wa mambo ya nje wa Japani Fumio Kishida alisema na ninamnukuu…Ikiwa ni nchi pekee iliyoathiriwa na mashambulio ya mabomu ya atomiki, ni azma ya nchi yetu kupeleka ujumbe wa madhara na machungu ya Hiroshima na Nagasaki kuvuka mipaka na vizazi..”

Naye Rais wa mkutano huo Balozi Mohammad Sabir Ismail wa Iraq pamoja na kutuma rambirambi kwa familia za manusura na wahanga wa mashambulio ya Nagasaki na Hiroshima amerejelea umuhimu wa kuundwa kwa kikundi cha kuandaa mpango kazi wa mkutano huo ili kuendeleza azma ya kutokomeza kuenea kwa silaha za nyuklia.

Bomu la atomiki liliangushwa na ndege ya kimarekani aina ya B-29 tarehe Sita Agosti 1945 huko Hiroshima na siku tatu baadaye tarehe Tisa Agosti bomu lingine la atomiki liliangushwa Nagasaki.