Baraza la Usalama lalaani shambulizi la bomu kwenye ubalozi wa Uturuki Mogadishu

29 Julai 2013

Wanachama wa Baraza la Usalama wamelaani vikali shambulizi la bomu la kujitoa mhanga kwenye jengo moja la ubalozi wa Uturuki mjini Mogadishu, Somalia, mnamo Julai 27, na ambalo lilisababisha kifo cha mtu mmoja na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama wameelezea huzuni yao na kutuma risala za rambirambi kwa familia za wahanga na kwa serikali na watu wa Uturuki.

Wamelaani vitendo vipya vya ghasia na vile vya mara kwa mara dhidi ya wawakilishi wa kidiplomasia na maafisa wa ubalozi, ambavyo huhatarisha maisha ya raia wasio na hatia, na kuzuia utendaji kazi wa kawaida wa maafisa hao wa ubalozi.

Wanachama hao wa Baraza la Usalama wamesisitiza kuwa ugaidi wa aina zote ni mojawapo wa tishio kubwa zaidi kwa amani na usalama, na kwamba vitendo vyovyote vya kigaidi ni vya uhalifu na haviwezi kukubalika, bila kujali sababu zake, vinafanyika wapi, au vinatekelezwa na nani.

Wameelezea haja ya kuwafikisha mbele ya sheria walotekeleza kitendo hicho, na kuahidi kuendelea kusaidia harakati za kisiasa  pamoja na amani na utulivu nchini Somalia.