Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali ya kibinadamu Syria

Baraza la Usalama lakutana kuhusu hali ya kibinadamu Syria

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili hali Mashariki ya Kati, ambapo pia limesikiliza taarifa za wakuu wa mashirika ya huduma za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Antonio Guterrs wa UNHCR na Valerie Amos wa OCHA, pamoja na Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu, Ivan Simonovic. Joshua Mmali ana maelezo zaidi(TAARIFA YA JOSHUA MMALI)

Mkutano wa Baraza la Usalama leo limezihusu mzozo wa Syria, na jinsi unavyouathiri ukanda mzima wa Mashriki ya Kati, zikiwemo nchi za Lebanon, Iraq na Uturuki.

Akilihutubia Baraza hilo kwa njia ya video kutoka Geneva, Uswisi, Mratibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA, Bi Valerie Amos, amesema hali tete ya kikanda iliyopo sasa, ambayo imetokana na mzozo wa Syria, ni hali inayohitaji kuitikiwa kwa njia ya kina na endelevu na jamii ya kimataifa.

(SAUTI YA VALERIE AMOS)

Madhara ya kiusalama, kiuchumi, kijamii, kisiasa kimaendeleo na kibinadamu yanayotokana na mzozo huu ni makubwa mno, na athari za kibinadamu haziwezi kukadiriwa, ukizingatia uchungu wa muda mrefu utokanao nao kwa kizazi cha sasa na cha siku zijazo. Mitandao ya familia na kijamii imesambaratika. Sifa ya Syria ya kuvumiliana imeharibiwa. Hatutizami tu uharibifu wa taifa, bali pia watu wake.

Naye Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuwahdumia Wakimbizi, UNHCR, Antonio Guterres, amesema idadi ya wakimbizi wa Syria katika ukanda mzima imefikia milioni 1.8, thuluthi mbili za wakimbizi hao wakiwa wamelazimika kukimbia makwao mwaka huu pekee, na kwa wastani watu elfu sita kila siku. Bwana Guterres amesema idadi ya wakimbizi kupanda hivi haijawahi kuonekana tangu mauaji ya kimbari nchini Rwanda, na kuelezea mateso wanayokumbana nayo wakimbizi hao.

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

Mzozo huu umeendelea kwa muda ambao haukutarajiwa, na madhara makubwa ya kibinadamu. Watu wa Syria wanaendelea kuteseka hata zaidi, mateso ambayo yameongezwa na joto la msimu wa kiangazi, na inahuzunisha hata zaidi katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Majirani za Syria wamekaribisha wakimbizi wengi wa Syria, na kuokoa mamia ya maelfu ya maisha. Lakini ukarimu huu una madhara yake. Matumaini ya suluhu la kisiasa na kumalizika mapigano bado hayapo, na ishara za kuathiri utulivu katika baadhi ya nchi jirani zinatia wasiwasi. Hali hii huenda ikazitumukiza matatani ikiwa jamii ya kimataifa haitachukua hatua mathubuti kuzisaidia.

Naye Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu haki za binadamu, Bwana Ivan Simonovic, amesema kati ya watu 92, 901 waliouawa, 6, 561 walikuwa watoto, 1,729 wakiwa chini ya miaka kumi.

(SAUTI YA IVAN SIMONOVIC)

“Watoto wameripotiwa kuzuiliwa, kuteswa, na kuuawa. Wamesajiliwa pia kama wapiganaji na makundi yenye silaha. Tume ya uchunguzi kuhusu Syria imeripoti kuwa yapata watoto 86 wameuawa wakipigana. Viwango vya juu vya mauaji vinavyokadiriwa kuwa watu elfu tano kila mwezi, vinaonyesha jinsi hali ilivyozorota katika mzozo huu.”