Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna mtoto anayepaswa kufa kwa sababu ya kwenda shule:Ban

Hakuna mtoto anayepaswa kufa kwa sababu ya kwenda shule:Ban

Mwakilishi Maalum wa masuala ya elimu katika Umoja wa Mataifa, Gordon Brown, amewashukuru familia ya Malala na madaktari ambao wamemwezesha Malala kuishi na kutekeleza yale ambayo wataliban walitaka asitekeleze. Bwana Brown amesema siku ya leo sio tu ya kusherehekea kuzaliwa kwa Malala na kunusurika kwake, bali ni siku ya kusherehekea mtazamo na ndoto yake:

(SAUTI YA BROWN)

Ndoto yake kwamba hakuna chochote, uwe upuuzi wa kisiasa, viwe vitisho au risasi za mwuaji, kinachopaswa kuwazuia haki ya kila mtoto, hususan wasichana na wavulana milioni 57 ambao wamenyimwa elimu, kuweza kwenda tena shuleni. Naamini kwamba leo tunaona uwezo mpya mkubwa duniani. Ni uwezo wa vijana kubadilisha ulimwengu na kuwezesha upatikanaji wa elmu kwa wote.”

Katika hotuba yake, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Vuk Jeremic, ameelezea kujivunia kwake kuwa kwenye jukwaa moja na Malala, na kusifu jinsi ambavyo amekuwa mfano kwa wengi wanaotetea haki zao za binadamu za kimsingi.

 (SAUTI YA VUK)

Leo tunasherehekea miaka kumi na sita ya kuzaliwa kwa msichana maalum na jasiri sana: Malala Yousafzai. Kuvumilia kwake ni ushahidi wa ujasiri wake, na ushahidi ulio hai kuwa vitendo vya mtu mmoja vinaweza kuleta matumaini kwa mamilioni ya waathiriwa wa ubaguzi na kutengwa. Elimu hulenga kuwawezesha watoto kunawiri wakiwa watu wazima, kama wazazi, wachuma riziki, viongozi wa kijamii na raia wanaowajibika, na kuwapa stadi, tabia na ufahamu watakaohitaji ili kuchangia jamii zao”

Naye Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon, amemshukuru mtoto Malala kwa kuamua kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake kwenye Umoja wa Mataifa…

(SAUTI YA BAN)

Malala alichagua kusherekea siku yake ya kuzaliwa na ulimwengu. Anatutolea wito tutimize ahadi zetu- tuwekeze katika vijana na kutanguliza elimu. Kwa kusherehekea siku hii maalum kwenye Umoja wa Mataifa, Malala anawaambia wengine kama yeye kote duniani kwamba hawapo peke yao. Serikali na wadau wamepiga hatua muhimu katika elimu. Lakini bado kuna kazi nyingi ya kufanya. Watoto milioni 57 hawaendi shuleni. Wengi wao ni wasichana. Nusu yao wanaishi katika nchi zenye mizozo. Hatuwezi kuacha hali hii iendelee. Hakuna mtoto anayepaswa kufa kwa sababu ya kwenda shule.”

Bwana Ban amesisitiza kwamba hakuna mahali popote ambapo walimu na watoto wanapaswa kuogopa kwenda shule, akirejelea lengo la mkakati wake wa kimataifa wa Elimu Kwanza.