Ukuaji mdogo wa uzalishaji wa kilimo watarajiwa: OECD-FAO

6 Juni 2013

Uzalishaji wa kilimo duniani unatarajiwa kukua kwa asilimia 1.5 kwa wastani kwa mwaka katika muongo ujao ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.1 kati ya mwaka 2003 na 2012.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Alhamisi na shirika la chakula na kilimo FAO na shirika la ushirikiano wa uchumi na maendeleo OECD.

Kupungua kwa ardhi ya kilimo, kupanda kwa gharama za uzalishaji, ongezeko la shinikizo la rasilimali na ongezeko la shinikizo la mazingira ni sababu kubwa za ukuaji mdogo wa uzalishaji wa kilimo. Lakini ripoti inasema usambazaji wa bidhaa za mashambani lazima uendelee kufuatana na mahitaji.

Mtazamo wa kilimo wa OECD na FAO kati ya mwaka 2013-2022 unatarajia bei kusalia za juu kiliko ilivyokuwa awali kwa mazao ya kilimo na bidhaa za mifugo kutokana na mchanganyoko wa ukuaji mdogo wa uzalishaji na mahitaji makubwa ikiwemo ya nishati ya mimea.

Ripoti inasema sasa sekta ya kilimo inaendeshwa na soko badala ya sera kama ilivyokuwa zamani. Imeongeza kuwa mapunguifu katika uzalishaji, kuyumba kwa bei na matatizo katika biashara vimesalia kuwa tishio kubwa la usalama wa chakula.