Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo la watu mashuhuri lakabidhi ripoti ya ajenda ya maendeleo baada ya 2015

Jopo la watu mashuhuri lakabidhi ripoti ya ajenda ya maendeleo baada ya 2015

Hatimaye jopo la watu mashuhuri lililoundwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon kuandaa mapendekezo ya ajenda ya maendeleo baada ya ukomo wa malengo ya maendeleo ya milenia mwaka 2015, leo limewasilisha ripoti hiyo mjini New York ambapo pamoja na mambo mengine limetambua amani, haki za binadamu na utawala bora kama kitovu cha maendeleo.Ripoti hiyo imewasilishwa na mmoja wa wajumbe wa jopo hilo Rais Susilo Bambag Yudhoyono wa Indonesia kwa Bwana Ban kwa niaba ya wajumbe wengine Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron.

Bwana Ban amesifu kazi ya jopo hilo hususan kwa kuweza kujumuisha mawazo kutoka pande mbali mbali kupitia mashauriano ya kina yaliyofanyikwa kipindi cha mwaka mmoja.

Amepongeza vile ambavyo wametambua kuwa ajenda baada ya mwaka 2015 ni lazima iwe jumuishi ikizingatia ubia, ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja na kwamba mipango iwe endelevu.

Katibu Mkuu amesema ripoti hiyo ni muhimu katika kuchangia mawazo ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 na tayari amempatia Rais wa Baraza Kuu nakala ya ripoti hiyo huku ikitarajiwa kuwekwa wazi kwa umma baadaye leo.