UNRWA yalaani shambulio kwenye kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Sbeineh Syria:

30 Mei 2013

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limearifiwa kuhusu mlipuko mkubwa kwenye kambi ya Sbeineh jimbo la Damascus nchini Syria hapo Mai 27 mwaka huu.

Ripoti za awali zinasema kwamba chanzo cha mlipuko huo ni shambulizi la angani au kombora, lakini hilo halikuweza kuthibitishwa kwani kambi hiyo bado haifikiki kutokana na mapigano yanayoendelea .

UNRWA imelaani vikali shambulio hiloambalo lilikatili maisha ya wakimbizi watano wa Kipalestina na kujeruhi wengine wanane, huku likisambaratisha makazi kadhaa ya wakimbizi .

Makambi ya wakim,bizi wa Kipalestina na mitaa ya jirani wanaendelea kushuhudia mapigano makali yanayoendelea nchini Syria na kujionea maisha ya watu na majeruhi kila uchao.

UNRWA inakadiria kwamba hadi sasa takribani wakimbizi wa Kipalestina 235,000 wamesambaratishwa na machafuko ya Syria , kambi ya Sbeineh yenyewe imetelekezwa kufuatia mapigano na miezi kadhaa ya kuvurumishwa makombora.

UNRWA imerejea kuitaka serikali ya Syria na majeshi ya upinzani kuzingatia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kuwalinda watu wake kwa kutoshambulia maeneo wanayoishi.