Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Iraq iko mbioni kusambaratika kama viongozi hawatochukua hatua kudhibiti machafuko:UM

Iraq iko mbioni kusambaratika kama viongozi hawatochukua hatua kudhibiti machafuko:UM

Ongezeko la machafuko nchini Iraq linaidumbukiza pabaya nchi hiyo na linachochea machafuko ya kidini endapo viongozi hawatochukua hatua za haraka kunusuru hali ameonya mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumza leo bwana Martin Kobler amesema wimbi la mashambulizi ya mabomu yaliyoukumba mji wa Baghdad leo, na kukatili maisha ya watu wengi huku gavana wa Anbar akiripotiwa kunusurika jaribio la mauaji baada ya mabomu kulipuka karibu na msafara wake na kujeruhi walinzi wake wanne.

Jaribio hilo limefuatia msururu wa mabomu mjini Baghdad Jumatatu yaliyokatili maisha ya watu zaidi ya 50.

Bwana Kobler ambaye pia ni mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa Iraq UNAMI, amelaani mashambulizi hayo dhidi ya msafara wa gavana. Jana akibadilishana mawazo na wabunge wa Ulaya ameelezea hofu yake juu ya ongezeko la ghasia na hatari ya taifa hilo kutumbukia kwenye vita vya kidini.