Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipango inahitajika kuwaandaa watoto kwa majanga: UNICEF

Mipango inahitajika kuwaandaa watoto kwa majanga: UNICEF

Kuna haja ya kuwa na mipango maalumu ya kuhakikisha watoto wanajua nini cha kufanya wakati janga likitokea. Hayo yamesemwa na bwana Anthony Spalton mtaalamu wa upunguzaji hatari ya majanga kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Bwana Spalton amesema watoto ni lazima washiriki mipango hiyo na waruhusiwe kutoa mtazamo wao wa kile wanachohisi kitawaweka salama.

Ameongeza kuwa watoto ni miongoni mwa kundi lililo katika hatari kubwa wakati wa majanga na hata miongoni mwa watoto wenyewe kuna wale walio katika hatari zaidi yaw engine mfano wale wenye ulemavu.

Bwana Anthony anahudhuria kongamano la nne la kimataifa la upunguzaji majanga linaloendelea mjini Geneva na kuhudhuriwa na wawakilishi wa serikali mbalimbali, jumuiya za kijamii, mashirika ya kimataifa, wanazuoni, taasisi za kiufundi na pia sekta binafsi.