Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bangladesh na Brazil zashinda tuzo la UN-Sasakawa

Bangladesh na Brazil zashinda tuzo la UN-Sasakawa

Nchi za Bangladesh na Brazil, ambazo hukumbwa zaidi na majanga ya mara kwa mara, zimepokea kwa pamoja tuzo la UN-Sasakawa, ambalo limewasilishwa na Mkuu wa Ofisi ya kupunguza hatari za Majanga katika Umoja wa Mataifa, Bi Margareta Wahlström, mbele ya mfadhili wa tuzo hilo na mwenyekiti wa Hazina ya Nippon, Yohei Sasakawa.

Bwana Sasakawa amesema kauli mbiu ya tuzo la mwaka huu ni “Kuchukua hatua ya pamoja”, ambayo Hazina ya Nippon ilianzisha baada ya tetemeko la ardhi na Tsunami mashariki mwa Japan, kwa kushirikiana na kampuni za biashara na mashirika yasiyo ya kiserikali kuandaa warsha za kuhamasisha kuhusu kuweka majengo yanayowarahisishia watu walemavu kujinusuru katika nyakati za dharura.

Tuzo hilo la thamani ya dola 20, 000 kwa kila mmoja, limetolewa kwa juhudi za Belo Horizonte, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Minas Gerais nchini Brazil wenye watu milioni 2.75, na ambao una maeneo 80 yenye hatari za mafuriko na ajali za udongo, pamoja na mkakati wa kitaifa wa kupunguza hatari za majanga nchini Bangladesh, ambao unajumuisha mashirika 10 ya kimataifa yasiyo ya kiserikali, na ambayo kwa pamoja yameonyesha ubunifu na ufanisi utokanao na ushirikiano.